IJUE VITA YAKO
UTANGULIZI:
Biblia hutueleza kuwa mkristo anayo vita anayopaswa kupigana katika maisha haya. Ingawa vita si jambo linawafurahisha watu wengi, hata hivyo biblia inasema kwa mkristo haiepukiki. Hii ni kwa vile Mungu anawatafuta washindi. Ni lazima adhihirishe kuwa watu wake wana uwezo zaidi kama ikilinganishwa na watu wengine wowote. Katika kitabu cha mwisho cha biblia Ufunuo tunaona Bwana Yesu akifurahi kuwapokea washindi kukaa nao milele.
Hata hivyo biblia hutuasa kuwa vita hii si ya jinsi ya kibinadamu yaani ya mwilini.
Efeso 6: 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
2 Wakorintho 10: 3 Ingawa tunaishi duniani lakini hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 Silaha za vita vyetu si za mwili, Bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. 5 Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo,
KUILEWA VITA YA KIROHO.
Kuilewa vita ni hatua muhimu kama utaweza kuishinda. Ndio maana katika dunia hii majeshi yote makini hutoa elimu ya vita. Unapojiandikisha tu kuingia jeshi unapimwa afya na kupekwa katika mafunzo ya awali. Hapo katika ukuruta (recruit) unafundishwa mambo ya msingi hasa nidhamu ya kijeshi na mbinu za vita. Baada ya kuhitimu hapo mafunzo zaidi ya kitaalamu ya jeshi hufuata. Katika elimu ya ufundi wa kivita (Military technology and equipment). Huko kuna elimu ya mawasiliano ya kivita, elimu ya ngome za kivita, roboti za kivita, zana za usafarishaji, mavazi ya kinga ya kivita n.k
Biblia inatufundisha kuwa aina ya vita ya kiroho ambayo ni tofauti na ile ya kimwili. Nayo vita ya kiroho ina shule yake ya kujifunzia vita.
Zaburi 18: 34 “Huifundisha mikono yangu kupigana vita, mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.”
Daudi alifundishwa na Mungu mwenyewe vita. Unaweza kuona alikuwa akiingia katika ulingo wa vita na maadui wa kidunia; lakini Daudi alikuwa juu yao wote. Mikono yake lipinda upinde wa shaba na akawafuatia maadui na kuwapata. Watu wengi walimwona Daudi kama mtu shujaa. Lakini Daudi alijua siri ya ushujaa wake ni Bwana.
Ukielewa vizuri nafasi yako katika vita ya kiroho, leo hii utatangaza vita juu ya vita ya shetani. Bado nakumbuka Nyerere alivyotangaza vita ya Kagera mwaka 1978. Nilikuwa nasikiliza redio akatoa hotuba akiwa Nachingwea “ …huyu mtu Amini, ameua watu wengi. Mtu huyu ni mshenzi, ameua watu wengi. Na sasa tutampiga. Uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo. Na sasa tutampiga!” Leo ufike mahali pa kumtangazia shetani sasa nitakushikisha adabu! Je utapambana vipi na maadui zako?
JE UNAWAJUA MAADUI UNAOPASWA KUWASHINDA?
Kama utafanikiwa vitani ni lazima umjue kwanza adui unayekabiliana naye na mbinu zake dhidi yako. Je unafahamu kuwa katika vita hii hupaswi kupambana na shetani? Hapo wengine mnagutuka, kama sikupambana na shetani nitapambana na nani!? Nami ndilo swali langu unamjua unayepaswa kupambana naye? Hatukuitwa kupambana na shetani. Yesu amepambana na shetani. Yesu alipokuja katika ulimwengu huu alisema huyu shetani ni saizi yangu. Aliwaacha kina Petro wakalala usingizi, alishughulikia tatizo hili yeye mwenyewe. Biblia yangu huniambia alichukua mwili ili afananishwe na hao aliotaka kuwatoa katika makucha ya shetani.
Waebrania 2:14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, Yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani, Shetani, 15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.
Tafsiri ya union version hutumia neno kumharibu badala ya lile la kumwangamiza. Je ina maana Yesu alikuja kumwua shetani? Tunajua hata mashetani alipomwona Yesu alishtuka na kung’aka; “umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” (Mathayo 8:29)hivyo neno kuharibu au kuangamiza hapa halina maana ya kuua. Tafsiri yake ya neno la kiyunani katargeo humaanisha:- isiyofaa (useless), zezeta (to be entirely idle),a kushindwa(fail), poteza (loose) fanya kuwa bure kabisa (bring to naught), ondosha (put away), tupu (void). Hivyo waweza kuona shetani amedhoofishwa mbele zako mithili ya simba mgonjwa aliye mahututi. Ingawa kwa wasiojua kilio cha maumivu ya simba mgonjwa huwafanya watimue mbio.
Angalia Wakolosai 2: 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili pamoja na amri zake, aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba Wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburuta kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba wa Kristo.
Biblia hutuonyesha kuwa Bwana Yesu katika kifo chake aliteka mateka. Mstari wa 15 anaposema “akiisha kuzivua enzi na mamlaka…” hapa hamaanishi alikuwa amevaa enzi na mamlaka, kisha katika hatua fulani akazivua katika mauti yake msalabani. Tafsiri ya biblia ya Amplified husomeka hivi “ (Mungu) alizinyang’anya enzi na mamlaka…zana zote za kivita (kama mateka) na kuzifanyisha hizo enzi na mamlaka gwaride la aibu linalodhihirisha kushindwa …” Kwa hiyo katika kifo chake, Yesu alivunja uwezo wote wa shetani juu yako. Aliteka kama majenerali wafanyazo vitani, na kisha akamvua adui silaha zake zote na kumdhalilisha hadharani kwa gwaride. Je wewe unashangilia unapoona maandamano haya; Bwana Yesu ametangulia na shetani akiwa peku peku bila mkanda, amevuliwa vyeo vyote, ameweka mikono kichwani na akizomewa kila mtaa maandamo yanakopita. Je unaogopa kuwa labda shetani akikuona unashangilia anaweza akakata kamba azizofungwa na Bwana Yesu akakukimbiza? Baadhi ya wakristo hufikiri hivi, Hawataki shetani awaone wakimzomea hata kama Yesu ametagulia mbele ya maandamano!
Hivi nikuulize swali, unaamini kweli kuwa Yesu alimshinda shetani. Na kuwa shetani tayari ameshindwa. Na sasa kama ameshindwa tayari je una vita ya kupambana naye? Bado utasema nina pambana na shetani? Nafikiri wakristo wengi vita yao dhidi ya shetani inafunua ujinga wa neno la Mungu uliomo ndani yao. Vita hiyo ni vita isiyokuwa ya lazima. Shetani alikwisha shindwa na Bwana Yesu.
Vita yetu sisi ni vita ya imani.
2 Timotheo 4:7.
7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimelinda.
Mtume Paulo akimwandikia Timetheo aliweka wazi aina ya vita waamini waliyo nayo. Paulo hakusema nimepiga shetani, lakini alisema imani nimeilinda. Vita yetu ni ya kulinda imani. Shetani atajaribu kuishambulia imani yako ili akufikie. Kinga uliyo nayo ni imani yako. Mtume Paulo katika Waefeso 6 anasema imani ni ngao inayozima mishale yote ya moto ya yule mwovu. Kwa hiyo tunajua vita mtume Paulo aliyopigana ilikuwa ya kulinda imani yake.
1 Timetheo 6:12,
12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.
Vita ya imani ndiyo vita uliyoitwa kupigana. Shetani hawezi kabisa kukugusa, wewe unalindwa mikononi mwa Mungu. Uhai wako umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Wewe tayari ni mshindi na zaidi ya mshindi. Haya yote yamefanikishwa na Yesu. Shetani anachoweza kufanya kwako ni kukuondolea imani yako. Ngao uliyopewa na Mungu ni imani yako. Shetani hawezi kupenya kama kuna imani. Hivyo anachojaribu kufanya ni kukunyang’anya imani yako. Hapo imani yako ikiondolewa utakuwa dhaifu kama wanadamu wote. Utakuwa mhanga wa matukio ya kila siku, utakuwa mhanga upepo unaovuma duniani. Kama ni magonjwa ya mlipuko nawe hutakosa, kama ni msimu wa ugumu wa uchumi nawe utakuwemo. Wasi wasi wa kutopata kabisa mwenzi nawe utakuwa nao. Hali mbaya zinazowatisha watu wote nawe zitakutisha! Kisa? Imani yako imepokonywa!
1 Petro 5: 8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu Ibilisi, kama simba angurumaye huzungukazunguka akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, siyo mpigeni bali mpingeni
Katika Petro neno linalosema mpingeni, humaanisha pia:- mkatalie, msikubaliane naye, msimfugulie njia, muwe na msimamo dhabiti dhidi yake. Vita unayopaswa kupigana ni ile ya kutunza imani kwa Mungu wako. Kuwa na uhakika kuwa kila alichosema ndivyo kitakavyo kuwa. Kujua kuwa Yesu anachosema juu yako kaatika biblia ndiyo kweli. Kulichukulia neno la Mungu kuwa ni sahihi.
Kwa mfano kama neno la Mungu linasema “ Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka” Warumi 10:9 unakubaliana na hilo neno katika maisha yako. Unasema kwa vile nimemkiri Yesu kwa kinywa change, nikimaanisha kabisa toka moyoni kuwa ndiye Bwana wa maisha yangu. Nimeamini kabisa kuwa Yesu alifufuka katika wafu. Hivyo nimeokoka. Sihitaji ushahidi zaidi, tayari neno la Mungu linatangaza kuwa nimeokoka, na ndivyo nilivyo! Haleluya nimeokoka. Lakini ukianza kusema zamani nilikuwa najisikia vizuri moyoni ila siku hizi sijui bado nimeokoka au la! Mbona majaribu yangu na shida zangu zimekuwa nyingi. Hivi kweli nimeokoka. Hapo tayari utakuwa njiani kushindwa maana imani yako juu ya wokovu imechukuliwa.
Au unasoma 1 Petro 2:24
“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Maneno haya haya yanatoka katika Isaya 53:5
“Bali alijeruhiwa kwa maskosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu, adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Na yamerudiwa Mathayo 8:17
“ ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya akisema. Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu. Na kuyachukua magonjwa yetu.”
Kutokana na maneno haya unaona Petro mwandishi wa mwisho katika mlolongo anatumia usemi wa wakati uliopita “na kwa kupigwa kwake mliponywa” sio mtaponywa au mnaponywa. Maana jambo lilikwishatendeka. Wakati mmoja nilipokuwa naomba juu ya jambo hili Roho mtakatifu alinionyesha kuwa mstari huu sio ahadi. Mstari huu wa 24 katika 1 Petro 2 ni ripoti ya tukio lililokwisha tendeka. Ni ukweli ulio katika kumbukumbu. Unaweza kukubaliana nao au ukaupinga lakini hautabadilika. Ni jambo lililokwisha tendeka. Faili limefungwa.
Unaweza kuanza kushindana na neno hili ukisema mbona sasa mimi bado sijapona? Unaweza kusema mambo haya yanasikika vizuri lakini ki matendo ni magumu. Lakini ukweli ni kuwa Yesu alipochapwa mijeledi na kujeruhiwa katika mwili wake akaumizwa, maumivu yale yalibeba maumivu yote ambayo yamekuwa yakiwatesa watu katika magonjwa. Tayari alikwisha yabeba. Na hapo kwa nini wewe uyabebe tena mara ya pili. Unaweza kufungua biblia yako na kusema hivi ndivyo nilivyo. Nimponywa pale Yesu alipopigwa katika kusulubiwa kwake. Magonjwa si sehemu ya maisha yangu. Nimeponywa kwa mapigo ya Bwana Yesu. Halleluya.
MAADUI WA IMANI YAKO.
Maadui unaopaswa kukabiliana nao ili kuilinda imani yako isipokonywe ni:-
1. MASHAKA JUU YA KILE MUNGU ANACHOSEMA JUU YAKO.
2. TARAJA
3. MAUNGAMO KINYUME NA UKWELI ANAOSIMAMA NAO KRISTO KAMA WAKILI
4. MATENDO YANAYOPINGANA NA IMANI YAKO
5. HOFU
Tutawaagalia maadui hawa mmoja mmoja na jinsi ya kukabiliana na kila mmoja wao kwa ushindi. Mtume Paulo alipambana nao wote akawashinda. Baada ya ushindi huu ndipo anasema “ 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimelinda.”
–Unity Christian Fellowship – Bukoba
Filed under: MAFUNDISHO
