“Utoaji ulio mwema ni mlango wa mafanikio na uponyaji wa kimwili, kiuchumi, na kiroho”
Dhabihu igusayo moyo wa Mungu ni mlango wa baraka yako.
Watu wengi wamekuwa wakitamani sana kubarikiwa na Mungu ila si wepesi kutaka kujua ni kwa namna gani au zipi ni kanuni za Mungu kwa mafanikio yao. Wengine kwa kutojua utaratibu wa Mungu wameamua hata kuvutwa na makanisa yanayotangaza kuwa wana ibada za kuombea watu Baraka na utajiri, ila Mungu yeye ni wa utaratibu na ukimgusa katika maeneo yake aliyoamuru yafanywe ni lazima utabarikiwa hata pasipo kuombewa na mitume na manabii, Ni muhimu sana kwa kila mtu kujifunza njia za Mungu na kujua ni kwa namna gani Mungu anawabarika watu wake.
Nyakati za leo ni rahisi sana kukuta mtu anamdai Mungu mambo mengi na Baraka ila ukitazama maisha yake jinsi yalivyo hakuna utoaji na si mwepesi kufanya mambo yanayobariki moyo wa Mungu.
Vipo vitu vinavyougusa moyo wa Mungu moja kwa moja, na vipo vitu vinafanyika na vimebeba sura nzuri ila si vyote vinavyougusa moyo wa Mungu. Katika sadaka kuna sadaka inayougusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kuna dhabihu itolewayo katika madhabahu ya Mungu ila haina sifa ya kugusa moyo wa Mungu.
Maandiko matakatifu yanatueleza kuwa utoaji ulio wa moyoni pasipo kushinikizwa ni sababu ya watu kubarikiwa na pia kukosa roho ya utoaji ubaki kuwa sababu ya watu kutobarikiwa.
Kitabu cha Marko 5:30-32 “Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, na wewe wasema ni nani aliyenigusa?” Watu wengine waliokuwa katika eneo lile walimpapasa Yesu ila hakuona mguso wowote, tofauti ni kwa Yule mama ambaye aligusa kwa mguso wa kudhamilia ambao uligusa moyo wa Mungu moja kwa moja na ukamfanya Mungu aingilie kati suala la Yule mama na kumponya.
Si kila agusaye ana mguso wa kugusa moja kwa moja, kuna wengine wanapapasa tu ila hawagusi ila kuna wengine wanagusa kabisa mpaka wanatoa mshituko na muitikio wa tofauti kwa mguswaji, mpapasaji hana athari yoyote ile ila mgusaji anaathari kubwa sana, na mgusaji aweza patiwa mambo mengi sana kwa kule tu kugusa kwake.
Marko 12:44-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. 42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. 43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; 44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Suala si kutoa ila suala ni kutoa dhabihu igusayo moyo wa Mungu kwa moja kwa moja, mtu unayeweza kumpima kwa viwango vyako vya kawaida kuwa yuko chini sana ndiye anaweza kuwa mtu afanyaye mambo yanayougusa moyo wa Mungu na kumfanya ajisikie vizuri.
Aidha katika eneo la sadaka kuna watu wengi watatoa dhabihu zao kama wapapasaji, ila kuna mmoja atatoa dhabihu ambayo itaugusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kumfanya Mungu asiwe na kimya na ashuke na kusababisha uponyaji wa maeneo yote kwa huyo mtu.
Dhabihu itolewayo kwa moyo na kupenda mbele za Mungu uwa inasema na kumkumbusha Mungu mara zote kwa habari yetu na maisha yetu. Ni kweli kuwa maombi tuyaombayo uzungumza sana mbele za Mungu, ila dhabihu tuzitoazo kwa moyo zinapaza sauti njema sana mara zote mbele za Mungu huku zikimkumbusha Mungu kuwa imempasa hatubariki. Kweli kuna wakati aweza kaa kimya kabisa ila akitazama moyo wako wa kumtolea na kujitoa mbele zako ni lazima aitike na kufanya hata zaidi ya yale uyaombayo. Maandiko usema yeye ufanya zaidi ya yale tuyaombayo, ushawahi kujihoji ndani yako kuwa ni nini kinamshawishi afanye zaidi ya yale tuyatamkayo katika kuomba kwetu? Ni kweli kuwa kuna neema ila pia dhabihu uzitoazo zinadai ulinzi, uponyaji, utajiri na mali, na heshima mbele za Mungu kwa maisha yako.
Mfano Kornelio sadaka alizokuwa akitoa kuwasaidia watu wengi wenye shida zilifika mbele za Mungu na kumkumbusha Mungu kuwa inapaswa afanye jambo kwa mtu wake Kornelio.
Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. 4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama, BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali wala sadaka yake, Kaini akagadhabika sana, uso wake ukakunjamana.” Suala si kutoa tu ila suala ni kutoa dhabihu yenye kupendeza mbele za Mungu. Kaini alikuwa anatoa tena sana ila tatizo alikuwa anatoa ziada za vile alivyonavyo na tena si vile vizuri, nadhani hakufahamu kuwa, “kipimo kile kile upimacho ndicho utapimiwa”. Tofauti kwa Habili ni ya kuwa yeye alitoa kila kilicho bora mbele za Mungu, kile ambacho ni kizuri na chenye kupendeza ndicho alichochagua kumpa BWANA, maandiko yanaeleza kuwa Mungu aliikubali na kuipokea sadaka ya Habili na akaikataa sadaka ya Kaini.
Kama si mtoaji au unatoa sadaka mbovu usijadili sana kwa nini mambo yako hayako vizuri. Jawabu unalo kuwa Mungu anakubali sana sadaka itolewayo kwa moyo na yenye kupendeza.
Ni dhahiri kuwa kukosa roho ya utoaji na kuwa na tabia ya kumkadiria Mungu katika yale tuyatoayo ni sababu kubwa sana ya kutopokea baraka za Mungu.
Watu wengi sana huwa na tabia njema ya kupenda kutoa kama ilivyokuwa kwa Kaini na Habili, ila katika kupenda huko wengi hutoa ziada ya vile walivyonavyo na wakati mwingine uchagua vitu ambavyo wanaona kwao vimepoteza thamani na ndivyo uvitoa kwa wengine. Kutoa ziada ya vitu ulivyonavyo na kuchagua kibovu katika vizuri kamwe hakuwezi kugusa moyo wa Mungu hata akageuka kama alivyogeuka kwa mama Yule aliyemgusa.
Wengine usema kuwa mimi ninatoa sana ila naona kama sibarikiwi, jiulize kama unatoa kwa namna njema inayoweza kumgusa moyo wa Mungu.
Nakumbuka siku moja nikiwa nimesafiri kuelekea mahali pa faragha kwa ajili ya maombi binafsi, nikiwa huko nilipata mguso wa tofauti sana wa kutoa mavazi yote ya thamani niliyokuwa nayo nimpatie mtu wa Mungu ambaye nilimkuta katika eneo hilo, suala hili lilikuwa gumu sana, haswa ukizingatia nami sikuwa na mavazi mazuri na ya kupendeza zaidi ya yale, nilishindana na ile sauti ya kufanya jambo hili, ila mwisho nikaona ni vyema niitii ile sauti na kutoa, haikuchukua muda mrefu kuna mama mmoja alikuja nyumbani na kuleta nguo nyingi zaidi ya zile nilizotoa na kupata viatu vizuri, kwangu hii ni uaminifu wa Mungu asemaye, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa kifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa”
Dhabihu inayougusa moyo wa Mungu ni dhabihu inayouma katika moyo wa mwanadamu, yaani kutoa kitu ukipendacho na ukionacho kuwa bora kuliko vyote na wapenda kukitumia ila kwa ajili ya BWANA unaamua kutoa si jambo rahisi na kufanya hivyo ni ishara ya upendo sana kwa Mungu na huonyesha kuwa unamjua unayemtumikia. Yaani dhabihu ambayo yaweza kuugusa moyo wa Mungu hata wewe mwenyewe ukitoa unaona umetoa kitu mbele za BWANA na wakati mwingine hata nafsi yako yagoma kabisa kwa kuwa nafsi ina tabia ya kujipenda yenyewe.
Mwanzo 22:2 “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.” Mungu anamtaka Ibrahimu atoe mtoto pekee aliye naye na ampendaye, si jambo rahisi kwa watu walio wengi kufanya hivi. Kwa mfano huu ni sawa na umeangaika kupanga miaka mingi sana halafu unapata tu nyumba yako mwenyewe ukasikia Mungu anakuambia nataka utoe hiyo nyumba uliyonayo umpatie mtu Fulani, au umetembea muda mrefu sana kwa miguu halafu umepata gari zuri la pekee na ulipendalo sana halafu ukasikia Mungu anakuambia toa hilo gari umpatie mtu Fulani si jambo rahisi.
Kumtii Mungu ni jambo la msingi sana katika maisha yetu, akisema hata kama jambo ni gumu sana wewe tii tu kwa kuwa kamwe hafanyi jambo hili kumkomoa mwanadamu, ila yeye ufanya yote kwa utukufu wake na hili kumfanya mwanadamu afurahie wema wake. Kwa Ibrahimu ukiendelea kusoma utaona kuwa Mungu anamuambia kwa kuwa hakumzuilia mwanae pekee ni lazima ambariki.
Sauti ya Mungu wakati mwingine inakuja kinyume na wewe ulivyo na waweza jiuliza mbona mimi nina vichache sana kwa nini amechagua mimi nitoe na si wale wenye navyo, ila jawabu ni kuwa Mungu amekuheshimu na amechagua kukubariki ndiyo maana amekuchagua wewe kati ya wengi.
Kijana mmoja katika Mathayo 19:21-22 “Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, Nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. 22 Yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kutoa na kuacha unavyomiliki kwa ajili ya Mungu ni suala la kujikana, kwa yule kijana alipoambiwa atoe alivyonavyo awape maskini aliondoka kwa kuhuzunika na akaona kuwa Mungu hamtakii mema kwa kumuagiza kutoa vitu vyake, ila laiti angejua siri iliyomkuta Ibrahimu na mjane wa Sarepta basi angetoa naye kwa kuwa angepata maradufu ya vile alivyokuwa navyo.
Mfano mwingine ni kitabu cha 1 Wafalme 17:13-16 “Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. 15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilonena kwa kinywa cha Eliya.”
Kutoa si kuwa navyo vitu vingi sana ila hata vile vidogo ulivyonavyo Mungu anataka umtumikie navyo, mjane wa Sarepta alidhani kuwa kutoa kwa ajili ya mtumishi wa Mungu ni mpaka awe na vitu vingi sana ila sivyo Mungu anavyotaka kwa watu wake. Kutoa ni moy na wala si wingi wa vitu ulivyo navyo.
Kutoa ni muhimu sana kwa kuwa ni kujiwekea hazina mbinguni ambapo nondo na kutu hawali, kama isemavyo katika Mathayo 6:19-21 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; 20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; 21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”
Kutoa mbele za Mungu unajiwekea hazina mbinguni mahali ambapo utakuwa ukiishi milele, mfano mmoja aliutoa mzee Moses Kulola kwa kusema “unakuta mtu anajisifu kuwa ana milioni kumi (10) benki ana mali nyingi sana ila hana hazina yoyote mbinguni na ni bahiri katika kutoa, ukimuuliza mtu huyu anaenda mbinguni, akifika bila shaka hata mahali pake kama atapata bahati hiyo hakutakuwa na hazina halizojiwekea.” Ukifahamu kuwa wewe duniani unapita kuelekea mbinguni weka juhudi katika siri hii pia. Kutoa katika hali ya kawaida ni kama kupoteza ila ni njia ya kujazwa vingi zaidi, ndiyo maana biblia usema kuwa “amfadhiliye/amsaidiaye maskini amkopesha BWANA”
Mungu anataka watu wake kujitoa kwa ajili ya kuifanya kazi ya injili na ana thamini sana wote wanaojitoa kwa ajili ya injili. Hagai 1, Na BWANA uumizwa sana na watu wanaothamini mambo ya nyumba zao na kusahau kazi ya nyumba ya BWANA.
Alisema nami mama yangu kuwa imenipasa kujisikia vibaya na kuona aibu sana pale napopendeza na kuonekana nipo vizuri sana huku wakitazama familia yangu na wazazi wangu hata kwa sehemu ndogo sana hatufananii, yaani nimewaacha mbali sana na hata aibu kutambulisha kuwa ni wazazi wangu. Lengo la nasaha hii kwangu ni kunihimiza kuwa nina wajibu wa kuwafanya wazazi wangu wang’ae na kupendeza hata watu wakitazama waone namna ninavyo jali.
Itaendelea sehemu ya pili
Na Mwl Kelvin Kitaso
Filed under: MAFUNDISHO
