“Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu” (Zaburi 141:3).
“Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!” (Mithali 15:23)
“7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake…. 20Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake” (Mithali 18: 7, 20).
“Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu” (Yakobo 3:2).
Nimesoma maombi ya Daudi kwa Mungu wake nikaona jambo la muhimu maishani mwa mwanadamu; Maneno ya kinywa!
Kumbe kuna uhusiano mkubwa kati ya MAFANIKIO ya mtu na MANENO yake? Naam, hili ni dhahiri, japo mara nyingi watu wanadhani kujinenea maneno ya laana tu ndio shida, kumbe, hata kunena jambo jingine hovyohovyo linaweza kuathiri hatma yako! Japo hukujilaani ila umefungua kinywa chako kwa upumbavu.
Basi nikaangalia na kuona jinsi ambavyo mara nyingi watu hufanya mzaha, na kufumbua vinywa vyao bila kufikiri, kumbe, maneno yao ni chakula chao! Wengi wana njaa hata sasa kwa sababu ya maneno yao tu!
Ndipo Daudi akaomba ULINZI wa Mungu kinywani mwake, naam, na mwanaye Suleiman akasema siri hii kwamba, “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake”.
Basi nikatazama tena nakujiuliza kwanini neno la kinywa liwe mtego? kwanini limkamate mtu na kumwangusha? Je! Utalipimaje kila neno kwamba lafaa? Nikaona mambo mawili: Kwanza, muda wa kulisema jambo (Mithali 15:23), na pili, kusudi la kulisema hilo jambo.
Kama UKAMILIFU wa mtu hupimwa kwa maneno yake (Yakobo 3:2), basi nikaona thamani katika maneno kama ilivyo katika matendo; yote mawili yanahitaji MLINZI ambaye ni Mungu. Lakini je! Waweza kulinda maneno na matendo bila kulinda mawazo ya moyo wako? Nikaona jambo hili, aliyefanikiwa kulinda MAWAZO ya moyo wake, ameweza vyote.
Frank P. Seth
Filed under: MAFUNDISHO
