Quantcast
Channel: MAFUNDISHO – Strictly Gospel
Viewing all articles
Browse latest Browse all 46

Ukombozi sio tukio ni safari!!

$
0
0
Pastor Carlos Kirimbai.

Kuna wimbi kubwa sana la huduma za ukombozi ambalo limeibuka katika siku za hivi karibuni. Zingine ni halisi lakini nyingi sio hata kidogo. Sasa sio nia ya post hii kuhukumu huduma ya mtu maana sina mamlaka hiyo ila ni nia ya post hii kusaidia japo kwa sehemu kuwa na msingi wa kimaandiko kwa ajili ya huduma ya ukombozi. Nisingependa kuingia katika unaga ubaga wa kama ukombozi ni sahihi kwa walio okoka au la ila ningependa kuweka chini msingi wa kimaandiko wa huduma ya ukombozi. 

Ninaposoma maandiko, kwanza kukombolewa ni jambo ambalo limewekwa ndani ya package ya wokovu.

Pia huu ukombozi sio jambo ambalo linatokea tu mara moja bali ni jambo ambalo linajidhihirisha katika maisha ya mtu kwa kadiri anavyokua katika kuijua kweli na kutembea katika hiyo.

Yesu alisema maneno haya:

Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. (YN. 8:31, 32 SUV).

Yesu alikuwa anasema na watu waliyomwamini. Ukisoma alichowaambia ni wazi kuwa Yesu alikuwa anadhihirisha kuwa kumwamini ni mwanzo tu wa safari. Yale uyafanyayo baada ya kumwamini ndo yanaamua ubora wa maisha katika Yeye utakayofurahia. Ukimwamini alafu huendelei katika neno Lake kuna kiwango cha uhuru katika Yeye hutafurahia. Na ni wazi huu uhuru anaouzungumzia hapa hauji kwa njia ya kumwamini tu bali unakuja kwa njia ya kuijua kweli Yake na kuiishi pia.

Sasa wengi wetu katika huduma ya ukombozi tunawafunza tu watu kufunguliwa na vifungo vya adui, kuvunjiwa laana nk bila ya kuweka msisitizo wa kuishi maisha ya kulisoma neno na kuliishi neno. Yesu aliweka wazi TUTAIJUA KWELI NA HIYO KWELI ITATUWEKA HURU. Uhuru wowote unaokuja katika maisha ya mwamini unatunzwa na kweli aijuaye na kuiishi. Sasa sijajua katika huduma za ukombozi kama msisitizo huo unawekwa. Maana watu wanaenda tu kuombewa ambayo sio mbaya lakini hawawajibiki binafsi na maisha yao na matokeo yake huduma ya ukombozi badala ya kuwasaidia ndo inawaharibu.

Kwanini nasema hivyo.

Soma haya maneno ya Yesu hapa:

Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya. (MT. 12:43-45 SUV).

Sio mimi nimesema maneno haya. Ni Yesu ndo kayasema. Pepo likishatolewa kwa mtu kwa njia ya huduma ya ukombozi, litaenda alafu kuna siku litarudi. Kama huyu mtu aliyetolewa mapepo hajajua jinsi ya kujipanga anaweza akawa amejiweka katika hali ya hatari sana. Kinachomfanya pepo arudi alipotoka ni pale ajapo na kukuta nyumba imefagiwa na kupambwa lakini tupu. Ni ule utupu wa maisha ya mtu ndo unamweka katika hali ya hatari sana. Kinachoweza kujaza maisha ya mtu sio maombi endelevu na huduma endelevu ya ukombozi ni neno la Mungu na neno la Mungu peke yake.

Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. (KOL. 3:16 SUV).

Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. (ZAB. 119:11 SUV).

Hatuwezi kukwepa wajibu wa kulijaza neno la Mungu ndani ya maisha yetu.

Na halijai kwa kulisoma tu linajaa kwa kulisoma na kuliishi.

Sijui kama tunaona jinsi ilivyo hatari kufunguliwa kwa njia ya maombi peke yake bila msisitizo kuwekwa katika maisha ya usomaji na kuliishi neno.

Hali ya mwisho ya huyu muathirika au mhanga ni mara saba mbaya kuliko ya kwanza.

Katika agano la kale ambalo ni kivuli cha agano jipya, Mungu aliwaambia wana wa Israel maneno haya:

Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi. (KUT. 23:28-30 SUV).

Cjui tunaona hayo maneno. Mungu anasema hatawaondoa wote mara moja. Ukweli ni huu japo unauma. Huwezi tu kwenda mahali na matatizo yako yoooooote yakaondoka mara moja. Ondoa dhana ya kuwa nitaenda mahali kuombewa, kutolewa mapepo, sijui kufanyiwa ukombozi na matatizo yangu yataisha. Mungu mwenyewe anasema hatayaondoa mara moja maana akifanya hivyo wanyama wa bara wataongezeka kukusumbua. Yaani ni kama kuyaondoa matatizo yote mara moja ni kufungulia matatizo makubwa zaidi. Yeye anaahidi kuyaondoa kidogo kidogo kwa kadiri sisi tunavyoongezeka na kuirithi nchi aliyotupa au ahadi alizotupa. Kuongezeka katika kimo ni muhimu mno.

Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; (1 PET. 2:2 SUV).

Kuongezeka au kuukulia wokovu ni matokeo ya neno na neno peke yake linaloingia maishani mwako kwa njia ya kulisoma, kufundishwa na hatimaye kuliishi. Ndipo unaanza kukua kiroho. Na matokeo ya kukua kiroho ni:

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli. (LK. 1:80 SUV).

Kwa kadiri unavyokua ndivyo unavyoongezeka nguvu rohoni.

Angalia maneno ya Paulo kwa wazee wa kanisa la Efeso:

Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. (MDO 20:32 SUV).

Neno la Mungu unapolisoma, kufundishwa na kuliishi ndilo linalokujenga na ndilo linalokupa urithinpamoja na wengine waliyotakasea kama wewe.

Tumeweka msisitizo mkubwa kuliko kwenye huduma ya ukombozi, kuvunja laana na kutoa mapepo bila ya kuweka mkazo wa kutosha katika kuwajibika binafsi katika kulisoma neno, kupata mafundisho sahihi na kuishi kila kinachofunuliwa kwetu tusimapo na tufundishwapo. Iko kama tunainua kizazi cha watu waliyookoka ambao hawapo tayari kulipa gharama ya kulijua na kuliishi neno ili kutembea katika ukamilifu wa uhuru ambao Yesu alienda msalabani kuununua kwa ajili yao.

Kila aliyeokoka ni mrithi pamoja na Yesu wa ahadi zote za Mungu. Lakini kama Paulo asemavyo:

Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; (GAL. 4:1 SUV).

Mrithi anapoendelea kuwa mtoto, hata afanyiwa huduma ya kufunguliwa kiasi gani, hata avunjiwe laana kiasi gani, hata atolewe mapepo kiasi gani, ataendelea tu kuwa kama mtumwa ingawa ni Bwana wa yote. Tumeitiwa kuwa bwana wa yote lakini adui mkubwa wa kutuzuia tusiyaone hayo sio mapepo, sio laana sio vifungo. Ni utoto. Na utoto ni matokeo ya kutoijua na kuiishi kweli.

Kama tunataka kuona ubora wa uzima ambao Kristo aliulipia pale msalabani ukiwa halisi maishani mwetu, tuache kukimbizana na huduma hii na ile na ile tukidhani kuna moja itaweka majibu yote mikononi mwetu tena kwa kuombewa tu na maombezi. Tulia mahali ambapo unajua Mungu amekuweka, tia mizizi yako chini hapo na kua katika kumjua Yeye na utaona uhru wako ukiachiliwa katika maisha yako hatua kwa hatua.

Nimalize kwa maneno haya ya Yesu:

Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. (MT. 24:26-28 SUV).

Yesu hapa anatuonya kuhusu kichaa kitakachoibuka siku za mwisho za watu kuambiana yupo huku, au kule au pale. Yesu keshasema tusiwasadiki. Alafu akasema maneno magumu sana ambayo sijui kama huwa tunayaelewa, akasema palipo na mzoga, tai hukusanyika. Kiswahili chetu hakikutenda haki hapa. Maana isemapo tai unaweza haraka ukafikiri ni yule ndege kwa kiingereza tunamwita eagle lakini ndege anayetajwa hapa ni vulture ambaye ni ndege ambaye anasekiaga harufu ya mizoga au kuna namna anajua mnyama anapokaribia kufa alafu wanasogea. Hawa ndege hawali vilivyo hai. Wanakula tu vulivyokufa. Ni mbaya sana mzoga unapokusanya na bahati mbaya mzogo haukusanyi ila ndege na wanyama waliyo maarufu kwa kula mizoga. Huko kukimbia kimbia kwako usije ukawa msaka mizoga.

Sasa kusema hivyo haimaanishi kuwa kila palipo na uwingi wa watu kilichowakusanya ni mzoga. Hapana. Kuna huduma nyingi kubwa nazijua ambazo zimekusanya watu kwa sababu ya kitu cha kipekee cha kiMungu kilichopo hapo na watu wanakifuata. Ila pia zipo nyingi zinazojiita “huduma” ambazo zinakusanya kwa sababu ni mzoga unaovutia tai.

Mzoga ni mrahisi sana kuujua. Unatoa harufu mbaya.

Asomaye na afahamu.

Pastor Carlos Kirimbai

……………………………………………………………..

Mafundisho mengine yanayokubali Kufunguliwa yaliwahi kujadiliwa bila kupata majibu sahihi

http://strictlygospel.wordpress.com/2011/09/08/kufunguliwa-kutoka-katika-ndoa-ya-mapepo-au-majini-mahaba/

http://strictlygospel.wordpress.com/2013/07/22/balaa-laana-na-mikosi-ya-kifamilia/


Filed under: MAFUNDISHO

Viewing all articles
Browse latest Browse all 46

Trending Articles